Home » Aliyekuwa Katibu Mkuu Wa Chadema Adai Katiba Mpya

Aliyekuwa Katibu Mkuu Wa Chadema Adai Katiba Mpya

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama kuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, Dkt. Wilbroad Slaa, ameunga  juhudi za kutaka mageuzi ya katiba.
Dkt. Slaa ambaye aligombea urais bila mafanikio mwaka 2010, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema kuanzia mwaka 2004 hadi 2015, alipostaafu kutokana na uamuzi wa chama hicho kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Karatu, ambapo alianzia safari yake ya kisiasa miaka minane baada ya kuacha siasa, Dkt. Slaa aliahidi kushirikiana na Chadema katika kudai katiba mpya, ambayo alisema ni suluhisho kwa matatizo mengi yanayowakabili wananchi.
Mkutano huo uliofanyika katika Kata ya Rhotia ulilenga kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo mgogoro wa maji katika mji wa Karatu.
Alipotolewa nafasi ya kusalimia wakazi wa Karatu, Dkt. Slaa alipongeza sera nzuri za Chadema.
Alisema katika harakati mbalimbali za Chadema, anaamini chama hicho kimekomaa na sasa kina uwezo wa kuongoza nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Mwanasheria Samuel Welwel alisema walimpa Dkt. Slaa nafasi tu ya kusalimia wakazi na wamemualika kwenye mkutano wa wadau wa maji siku ya Jumatatu Karatu.
Hata hivyo, alisema chama hicho bado hakijampokea rasmi kurudi Chadema, na ikiwa kuna utaratibu wa aina hiyo, suala hilo litafanywa na viongozi wa kitaifa.
Lakini Dkt. Slaa mwenyewe aliwahi kusema kuwa si mwanachama wa chama chochote cha kisiasa, na licha ya hilo, ataendelea kutoa maoni na ushauri wake kuhusu masuala mbalimbali yenye manufaa kwa taifa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!