Home » KMPDU Yafichua Jinsi Ukosefu Wa Likizo Unaathiri Madaktari

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) umetoa wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa idadi ya madaktari wanaojitoa uhai nchini Kenya.

Katika taarifa muungano huo umefichua kuwa taifa tayari lilikuwa limepoteza madaktari saba katika muda wa miaka miwili iliyopita.
Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah, ametaja visa hivyo vya kujitoa uhai na hali duni ya kazi.

Muungano huo umeeleza ukosefu wa siku za likizo kama mojawapo ya masuala muhimu yanayosababisha kuongezeka kwa visa vya kujitia kitanzi miongoni mwa madaktari.

Dkt Attellah alizidi kulaumu malipo duni kuwa sababu nyingine inayowasukuma madaktari wa Kenya kujitoa uhai.
Muungano huo aidha umelaumu serikali kwa kutoheshimu Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) unaoelezea malipo ya kimsingi na marupurupu ya madaktari.

KMPDU imekashifu zaidi kusita kwa serikali kuajiri madaktari zaidi ikitaja kuwa ilisababisha kukithiri kwa mfumo huo na kuwafanya madaktari wanaohudumu kuzama katika mafadhaiko.

Ikumbukwe kuwa Muungano huo ulikuwa umetishia kugoma mnamo Desemba 23, 2022, kutokana na hali mbaya ya kazi.
Mnamo Januari 4, mwaka huu, katika mkutano ulioleta pamoja Wizara ya Afya, Baraza la Magavana, na maafisa wa KMPDU, mgomo huo ulizuiliwa baada ya wahusika kukubaliana kukagua CBA iliyopo.

Madaktari hao walishutumu Wizara ya Afya wakitaja ukosefu wa nia njema kutoka kwa serikali kushughulikia changamoto zinazowaathiri.
Ufichuzi huo na KMPDU ulitolewa siku moja baada ya Muungano wa Maafisa wa Kitabibu nchini Kenya kuapa kupunguza zana zao kwa kile walichokitaja kama kupuuzwa na serikali.

Kulingana na wafanyikazi wa afya, utambuzi wa polepole wa huduma ya afya kwa wote, ubaguzi katika malipo ya mafunzo, na ukosefu wa kikosi kazi cha kitaifa cha afya ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!