Home » Absalom Odhiambo Kusalia Korokoroni Kwa Siku Moja Zaidi

Absalom Odhiambo Kusalia Korokoroni Kwa Siku Moja Zaidi

Mwakilishi wadi wa Korogocho Absalom Odhiambo amefikishwa kortini leo hii Jumanne baada ya kukamatwa hiyo jana Jumatatu.

Mwakilishi wadi huyo anadaiwa kutoa maneno ambayo kwa mujibu wa polisi “yana uwezekano wa kusababisha vurugu au kuyumbisha Taifa.”

Polisi wanasema Odhiambo alitamka maneno hayo yanayodaiwa kuwa ya uchochezi wakati wa mkutano wa Azimio la Umoja uliofanyika katika uwanja wa Kamukunji mnamo Jumatatu, Januari 23.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI sasa ameiomba mahakama kuwapa muda wa siku saba kumzuilia Odhiambo ili kukamilisha uchunguzi.

DCI inadai kuwa wanahitaji siku saba kupata jumbe zozote za uchochezi kutoka kwa simu yake na kurekodi taarifa ili serikali kuongeza ushahidi kwa upande wa mashtaka.

Hata hivyo, mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Danstan Omari wamepinga ombi hilo wakisema kuwa Odhiambo si mhalifu na kwamba kushtakiwa kwake kumechochewa kisiasa.

Odhiambo sasa atasalia mikononi mwa polisi huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi wake kesho jumatano.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!