Home » Gavana Mutula Junior Kufanya Kazi Na Serikali

Gavana wa kaunti ya Makueni Mutula Kilonzo Jr ameahidi kutojihusisha na mikutano na maandamano yoyote ya Azimio.

Akizungumza huko Makueni, Mutula Jr, ambaye alichaguliwa kwa tikiti ya chama cha kidemokrasia cha Wiper, amesema hatajihusisha na mikutano hiyo hadi eneo la Ukambani lipate miradi ya maendeleo kama vile eneo la Nyanza.

Mutula amesema kwa sasa atashirikiana na serikali iliyopo madarakani kuhakikisha inawafikishia wananchi wake maendeleo, akieleza kuwa kupigana na serikali ya sasa hakutasaidia jamii ya Wakamba.

Aidha amedaia kuwa eneo la Ukambani si sawa na Nyanza katika masuala ya maendeleo na ni wakati mwafaka wafungue maendeleo sawa na yale ya Nyanza badala ya kushiriki maandamano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Mutula, ambaye ni makamu mwenyekiti wa chama cha demokrasia cha Wiper kilicho katika muungano wa Azimio, huenda akazozana na kiongozi wa chama hicho Stephen Kalonzo Musyoka ambaye amekuwa mstari wa mbele kushiriki mikutano ya Azimio.

Mutua amewahi kusema bila hofu kuwa licha ya kuchaguliwa kwa tikiti ya Wiper alikuwa tayari kufanya kazi na serikali ya sasa.

Mwaka jana, aliwataka viongozi wa eneo la Ukambani kuhakikisha wanafanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza kwa manufaa ya watu wao.
Mutula alieleza kuwa Ukambani haiwezi kuwa katika upinzani kila mara, akiwataka viongozi kufikiria mahitaji ya watu wao.

Magavana watatu wa Ukambani ambao wote walichaguliwa kwa tikiti ya chama cha Wiper wanaonekana kufanya uamuzi wa kufanya kazi na Kenya Kwanza licha ya kiongozi wao wa chama kuwaongoza kwa upinzani.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!