Walimu 25 Wamesafirishwa Kwa Ndege Ya Kijeshi Hadi Shuleni

Walimu 25 wanaofanya kazi katika shule za msitu wa Boni katika kaunti ya Lamu wamesafirishwa kwa ndege ya kijeshi hadi katika taasisi zao.
Kikosi cha mashirika mbalimbali ya usalama cha Operesheni ya Amani Boni (OAB) kikiongozwa na Kikosi cha Ulinzi cha Kenya (KDF) kimechukua usukani wa usafirishaji wa walimu hao na mizigo yao kurudi katika maeneo yao ya kazi kutoka Uwanja wa Ndege wa Mokowe.
Shule za msingi za Mangai, Mararani, Milimani, Basuba na Kiangwe zilikuwa zimefungwa kwa wiki moja baada ya walimu hao kukosa kuripoti katika taasisi hizo kutokana na changamoto za usafiri.
Mkurugenzi wa Elimu wa Lamu Joshua Kaaga ameshukuru mashirika ya usalama kwa juhudi zao katika kuhakikisha wanafunzi zaidi ya 400 katika msitu wa Boni wanaanza tena kusoma kama wakenya wengine.
Kaaga amesema afisi yake itaendelea kushirikiana na idara ya usalama ili kuhakikisha shughuli za elimu katika maeneo yote ambayo ni magumu kufikiwa ya Lamu, haswa msitu wa Boni, yanafanyika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Kuajiri Walimu Kaunti ya Lamu Riziki Daido, amesema angalau walimu 30 zaidi wataajiriwa kuhudumu katika shule za msitu wa Boni katika shughuli ya kuajiri walimu inayoendelea.
Aidha Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu Charles Kitheka amewahakikishia wakufunzi wanaofanya kazi katika msitu wa Boni kwamba usalama wao umehakikishwa.
Hatua ya vyombo vya ulinzi na usalama kuwasafirisha kwa ndege walimu hao kwenda shule za msitu wa Boni, inafuatia ziara ya hivi karibuni ya maafisa wa mashirika mbalimbali ya Operesheni Amani Boni, wakiongozwa na Meja Jenerali Mkuu wa Kamandi ya Mashariki, Juma Mwinyikai.
Ziara hiyo ililenga kushughulikia maswala ya wenyeji kuhusu hali ya usalama, afya na elimu.
Katika ziara hiyo, Meja Jenerali Mwinyikai aliahidi kushirikiana na ofisi ya elimu na wadau wengine kuhakikisha kunatolewa chopa ya kijeshi kuwasafirisha walimu hao kurudi msitu wa Boni haraka iwezekanavyo.