Koigi Wa Wamwere Apongeza Rais Na Naibu Wake
Mbunge wa zamani wa Subukia Koigi Wa Wamwere amepongeza juhudi za haraka za rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kumtoa Mukami Kimathi hospitalini baada ya kuzuiliwa kutokana na kutolipa bili ya milioni 1.3.
Wakati huo huo, amewataka viongozi hao kukumbuka mashujaa wengine waliopigania uhuru wa kwanza na wa pili.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Koigi amesema wito wa Gachagua kuwataka walionyakua mashamba kuyatoa kwa mashujaa halisi ni wa kupigiwa upato pia.
Aidha, amemtaka naibu wa rais kuhakikisha serikali ya Uingereza imefichua walikomzika Field Marshal Dedan Kimathi na mashujaa wengine wa Mau Mau waliozikwa kwa siri.
Koigi anasema naibu rais pia anapaswa kuiomba serikali ya Uingereza kurudisha kichwa cha shujaa Koitalel Arap Samoei nchini Kenya kama vile Wabelgiji walivyorudisha jino la Patrice Lumumba nchini DR Congo.