Home » Malumbano Mapya Yaibuka Meru

Malumbano mapya ya uongozi yameibuka katika Kaunti ya Meru, huku ya hivi punde ikiwa kati ya Gavana Kawira Mwangaza na naibu wake Isaac Mutuma, pamoja na viongozi wengine walioteuliwa na gavana huyo.

 

Kwa muda wa wiki moja sasa, Mwangaza na Mutuma wameonekana kwenye njia panda baada ya gari moja rasmi la naibu gavana kubatilishwa na msaidizi wake kufukuzwa kazi baadaye.

 

Inadaiwa kuwa hii ilikuwa baada ya Mutuma kukosa kujibu wapinzani wa Mwangaza wakati wa hafla ya mazishi wiki jana.

 

Ijapokuwa hakuna aliyejitokeza hadharani kupunguza tofauti hiyo, katibu wa kaunti, msaidizi wa gavana na kamati kuu ya kaunti tayari wamemkashifu naibu gavana huyo kwa kutotekeleza majukumu yake ikiwemo kutohudhuria vikao vya baraza la mawaziri.

 

Wawakilishi wa wadi, wakiongozwa na naibu spika na kiongozi wa wachache, wanasema wamekatishwa tamaa na uongozi wa Gavana Mwangaza, miezi mitano tu baada ya jaribio la kumwondoa madarakani.

 

Wamemtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kuelekea kaunti hiyo na kutatua mzozo huo ambao wanahisi ni mbaya zaidi kuliko ule wa awali na kuashiria zaidi mpango mwingine wa kumtimua Gavana Mwangaza.

 

Huku serikali ya kaunti ikiunga mkono ombi la kufutilia mbali bodi ya utumishi wa umma kaunti hiyo kwa misingi kwamba haikuundwa vyema, wawakilishi wa wadi hao wako upinzani.

 

Wanasema kuwa ikiwa bodi hiyo imekuwa ikihudumu kinyume na sheria kwa zaidi ya miaka sita sasa, wale walioajiriwa katika kipindi hiki wanapaswa kufukuzwa pia.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!