Polisi Wamsaka Mwanaume Aliyewafunga Watoto Minyororo
Maafisa wa polisi katika eneo bunge la Mumias kaunti ya Kakamega wanamsaka mwanamume mwenye umri wa miaka 45 kwa jina Simon Mila Alichi ambaye aliwafungia watoto wake wawili katika chumba kimoja na kuwafunga kwa minyororo.
Watoto walifungiwa chumbani mchana na usiku, bila chakula cha kula.
Kulingana na wazazi wa mshukiwa John Mila na Ruth Andayi, wajukuu wao walikuwa wamefukuzwa shule na kufungiwa chumbani kimya na baba yao, ambaye aliachana na mkewe takriban miaka miwili iliyopita.
Majirani zake, wakiongozwa na Nicholas Nandwa, wanasema mshukiwa huyo amekuwa akiwaoa wanawake wengine na kuwataliki ndani ya muda mfupi. Wanamuelezea kuwa ni mtu anayeishi maisha ya siri.
Akithibitisha kisa hicho, chifu msaidizi wa Lokesheni Ndogo ya Maraba Benson Ochango aliwanyooshea vidole majirani kwa kukosa kuripoti tukio hilo kwa wakati.
Watoto hao wamepelekwa katika makao ya watoto huko Mumias, wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu yeyote atakayepewa malezi.