Home » Kuria Ataja Upangaji Uzazi Kama ‘Mpango Potovu’

Waziri wa Biashara Moses Kuria amekashifu ‘mpango potofu’ ya kupanga uzazi akisema ni lazima kuwe na ukaguzi wa wazi ili familia ziendelee kuwepo bila udhibiti.

 

Akizungumza alipofungua rasmi Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kenya jijini Nairobi hii leo Jumatatu, Kuria amesema kuwa nchi za G-20 zimeendelea zaidi kutokana idadi ya watu wala si rasilimali zao.

 

Kuria ametoa mfano wa nchi ya Indonesia aliyoitembelea hivi karibuni, akisema ndiyo nchi inayoshika nafasi ya 15 kwa uchumi duniani ikiwa na dola trilioni 1.8 ambazo ni sawa na pato zima la Afrika.

 

Kulingana na Kuria, Indonesia ndipo ilipo katika maendeleo kwa sababu ‘imetumia vyema wakazi wake milioni 300.’

 

Matamshi yake, hata hivyo, yanaweza kuchochea hisia nyingi kutoka kwa watetezi wa upangaji uzazi.

 

Kauli yake inajiri wakati ambapo juhudi zimewekwa ili kuhakikisha nchi inapata huduma zinazofikiwa, za usawa na bora za upangaji uzazi bila mahitaji ambayo hayajatimizwa ifikapo 2030.

 

Aidha, wataalamu wa afya wanaonya kuwa kushindwa kudhibiti idadi ya watu kwa sasa kuna uwezekano wa kuifanya serikali kuchukua tahadhari mbaya ya kuwa na idadi kubwa ya watu katika siku zijazo.

 

Chini ya wiki mbili zilizopita, Rais William Ruto aliwahimiza wanawake wa Njambini kaunti ya Nyandarua kukumbatia upangaji uzazi baada ya ripoti kuwa eneo hilo lilikuwa linaongoza kwa uzazi.

 

Alikiri kuwa serikali imekuja na mpango wa uzazi wa bure maarufu kwa jina la Linda Mama ili kuwaepusha na gharama za hospitali lakini akasema wajifungue kwa wastani.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!