Watu Tisa Wafariki Marsabit

Watu tisa wamefariki baada ya kuzuka kwa ugonjwa usiojulikana ambao umeikumba kaunti ya kaskazini ya Marsabit katika muda wa wiki mbili zilizopita.
Mamlaka husika zinasema zaidi ya watu wengine 80 ni wagonjwa mahututi baada ya ugonjwa huo kusambaa katika eneo la Kargi, Kaunti Ndogo ya Loiyangalani.
Aidha Vifo vingi vinasemekana kutokea katika maeneo ya malisho, maarufu kwa jina la Foras.
Uchunguzi wa awali kutoka kwa maafisa wa afya unaonyesha kuwa huenda ikawa ni aina ya malaria kali kwani wagonjwa wanasemekana kuwa na macho ya manjano, wengu kuvimba, maumivu makali ya kichwa, na dalili za mafua.
Malaria imeenea katika Eneo bunge la Laisamis kwa muda mrefu sasa.
Idara ya afya kaunti ya Marsabit imesema kwenye taarifa hii leo kwamba timu ya wataalam wa uchunguzi wa magonjwa na wataalamu wa maabara iko mashinani kubaini chanzo cha mkurupuko huo.