Rais Ruto Atetea Kukata Wakenya Asilimia 3 Ya Mshahara Wao
Rais William Ruto amesema kuwa mpango wa Hazina ya Makazi wa asilimia 3 wa nyumba za bei nafuu ndio njia pekee ya kuwawezesha watu wa kipato cha chini kumiliki nyumba hizo.
Akizungumza katika uwekaji msingi wa Mradi wa Makazi ya Hifadhi ya Lapfund Bellevue jijini Nairobi, Mkuu wa Nchi amedai kuwa mpango wa nyumba wa bei nafuu ulikuwa ahadi ya kampeni ambayo alipaswa kutimiza.
Zaidi ya hayo, amewataka viongozi wa kisiasa ambao walikuwa kinyume na mpango huo, akisema kuwa wengi walifanya naye kampeni na kuwaahidi Wakenya nyumba za bei nafuu ambapo kwa sasa ni wakati wa kutekeleza.
Ameeleza kuwa kiasi hicho kitakatwa kwenye mshahara wa kila mfanyakazi na nyongeza ya asilimia 3 itakayochangwa na waajiri.
Rais Ruto amebainisha kuwa serikali ilikuwa na mipango ya kushirikisha wawekezaji ili kuhakikisha kuwa idadi ya nyumba zinazojengwa kila mwaka zimeongezwa katika mpango wa nyumba za bei nafuu.
Mnamo Jumatano, Aprili 25, Katibu Mkuu wa Nyumba Charles Hinga alifafanua kuwa makato ya asilimia 3 ya mishahara ya kila mwezi sio lazima kwa Wakenya wote.