Aaron Cheruiyot:Serikali Haitashiriki Mazungumzo Maandamano Yakiendelea
Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot ametoa wito kwa Muungano wa Azimio la Umoja kuchagua kati ya mazungumzo wa pande mbili Bungeni na maandamano.
Mwanasiasa huyo ameshikilia kuwa hakuna njia ambayo muungano tawala wa Kenya Kwanza unaweza kukubali kufanya mazungumzo na upinzani kunapokuwa na maandamano sambamba mitaani.
Seneta huyo wa Kericho ameeleza zaidi kuwa tangazo la Azimio la kuandaa maandamano sambamba na mazungumzo ya pande mbili lilionyesha kuwa upinzani ulikosa kujitolea kupata suluhu.
Matamshi ya Cheruiyot yanajiri siku moja baada ya timu ya wanachama saba ya Azimio inayoongozwa na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo kusisitiza kuwa mchakato huo hauwezi kuwa wa bunge kabisa, wakitaja wasiwasi wa ushiriki wa umma.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga, wakati wa mkutano wa aliofanya Nairobi jana Alhamisi alidokeza uwezekano wa kuanzisha tena maandamano mitaani baada ya kukamilika kwa mwezi wa Ramadhani.
Mkutano wa Azimio mjini Nairobi ulikuwa wa kwanza kati ya misururu ya mazungumzo ya umma iliyozinduliwa na Odinga ambayo alisema ililenga kuwafahamisha wafuasi wake kuhusu maendeleo ya ushirikiano na serikali.
Yakijiri hayo, rais William ruto amesema kwa sasa ni wakati wa maendeleo si maandamano kama yalivyotolewa na muungano wa azimio.
Rais amezungumza kule Mavoko katika kaunti ya Machakos baada ya kuzindua mradi wa maji safi yatakayotumika maeneo mbalimbali kama vile mlolongo,syokimau na Athi River