Wakili Wa Raila Aandikia ICC Barua, Aorodhesha Madai 9 Dhidi Ya Serikali
Muungano wa Azimio la Umoja one-kenya umeandikia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yenye makao yake makuu Hague, Uholanzi, kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu hali ya kisiasa nchini Kenya.
Katika barua iliyoandikwa na wakili Paul Mwangi, ambaye ni wakili wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Azimio imemshutumu Rais William Ruto kwa kudharau Katiba na Sheria za Kenya ,demokrasia na taasisi zake.
Mwangi ameorodhesha masuala tisa ambayo ameitaka ICC kuingilia kati ili kurejesha utulivu nchini.
Katika barua hiyo, viongozi wa azimio wamemshutumu vile vile Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome kwa kuunda kitengo cha polisi wahuni kuwalenga wafuasi wake wakati wa maandamano.
Azimio pia imearifu mahakama ya kimataifa kwamba Koome alishindwa kufuata Katiba kwa kupiga marufuku maandamano ya umma.
Suala la jaribio la kuuawa kwa kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga pia limeangaziwa kwenye barua hiyo.
Mwangi amebainisha kuwa maafisa wa kutekeleza sheria walipiga risasi 10 kwenye gari la Odinga karibu na eneo la Pipeline eneo bunge la Embakasi Kusini mnamo Jumatatu, Aprili 3 wakati wa maandamano.