Raila Adai Uhuru Kenyatta Hajihusishi Na Maandamano

Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja One-Kenya Raila Odinga amepuuzilia mbali madai kwamba rais wa zamani na mwenyekiti wa baraza la Azimio Uhuru Kenyatta, anafadhili maandamano ya upinzani dhidi ya serikali.
Kufuatia maandamano ya Jumatatu na ya pili katika mfululizo wa maandamano ya kila wiki mbili katika siku zijazo , Odinga ameshikilia kuwa Kenyatta hajihusishi na maswala ya maandamano ya Azimio, licha ya kuwa bado ni mwanachama.
Waziri Mkuu huyo wa zamani amelaani uvamizi wa Jumatatu kwenye kiwanda chake cha gesi cha East Africa Spectre Limited jijini Nairobi, pamoja na uvamizi wa ardhi kubwa inayomilikiwa na familia ya Kenyatta.
Wahuni walivamia ardhi ya familia ya Kenyatta kando ya Barabara ya Nairobi Eastern Bypass asubuhi, na kukata miti na kuwaondoa kondoo, saa chache kabla ya kampuni ya gesi ya Odinga kushambuliwa na madirisha kadhaa kuvunjwa.
Kulingana na kiongozi huyo wa upinzani, hii ni hatua iliyopangwa vyema na serikali ya kusambaratisha upinzani na kusema Kenyatta analengwa kwa sababu ya uanachama wake Azimio.
Wiki jana, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wah alionya hadharani kwamba ardhi ya familia ya Kenyatta inaweza kuvamiwa na wenyeji iwapo angeendeleza kile alichotaja kuwa kufadhili maandamano ya Azimio.
“Ninataka kumwomba rais wetu wa zamani kuheshimu mali ya watu wengine. Iwapo huwezi kufanya hivyo, tuna maswali mengi sana ya kukuuliza kuanzia ardhi unayoishi Ruiru, Taita Taveta, na Nakuru. Ukishambulia mali ya watu, pia tutashambulia ardhi yako na kuhakikisha wale ambao hawana ardhi wanapata,” alisema Kirinyaga.
Mbunge huyo baadaye alijitenga na uvamizi huo, akisema Jumanne kwamba maoni yake yalikuwa tu onyo kwa Kenyatta kuhusu kile wafuasi wake walikuwa wakisema kuhusu ufadhili wake wa maandamano ya upinzani.
Odinga mwenyewe amemshutumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kupanga mashambulio hayo.