Watoto Wawili Wazama Kwenye Sehemu Ya Chemichemi Huko Budalangi

Watoto wawili wenye umri wa miaka miwili na mitatu wamekufa maji walipokuwa wakicheza kwenye sehemu za chemichemi katika Wadi ya Bunyala Kaskazini, Kaunti ya Busia.
Christine Anyango na Simon Okochi walikuwa wakicheza kwenye sehemu hiyo walipokumbana na kifo chao.
Ndugu hao walikuwa wameachwa peke yao nyumbani wakati wazazi wao walipokuwa wakilima shamba kwa msimu wa upanzi.
Kulingana na chifu wa eneo hilo Jael Mudonga, wawili hao walienda kuteka maji kwenye sehemu hizo kabla ya kukutana na kifo chao.
“Watoto hao walikwenda kuteka maji kwenye sehemu za chemichemi kwa jirani yao asubuhi na kuanza kucheza kwenye maji kabla ya kuzama,” alisema.
Mudonga pia amewataka wazazi kutowaacha watoto wao karibu na vyanzo vya maji au kuwaruhusu kuteka maji pekee yao.
“Hili ni tukio la kusikitisha sana na ningependa kuwaomba wazazi kutoruhusu watoto kuchota maji peke yao,” chifu aliongeza.
Polisi wamechukua miili hiyo miwili hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Port Victoria huku wakianzisha uchunguzi.