Polisi Walazimika Kutumia Vitoza Machozi Kuwatawanya Waandamanaji
Polisi walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya waandamanaji katika maeneo kadhaa ya Nairobi na Kisumu wanaoandamana dhidi ya serikali siku ya Jumatatu wakitaka kushushwa kwa gharama ya juu ya maisha.
Hii ni baada ya upinzani kuapa kuwa maandamano yataendelea licha ya marufuku ya polisi.
Usalama ulikuwa mkali huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwa jijini Nairobi na kushika doria mitaa kadhaa ikiwemo Kibera,Mathare na Kawangware. Maduka mengi yalifungwa na huduma za treni kutoka viunga vya mji mkuu hadi wilaya kuu ya biashara zikisitishwa.
Kiongozi wa Azimio La umoja Raila Odinga pamoja na viongozi wengine wa upinzani wamewataka watu kujitokeza barabarani kila Jumatatu na Alhamisi, hata baada ya maandamano wiki moja iliyopita kuwa na vurugu na kulemaza shughuli za jiji la Nairobi.
Polisi walikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe katika kitongoji duni kikubwa cha Nairobi cha Kibera, ambapo waandamanaji walichoma matairi, wakikaidi onyo la Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome ambaye alisema Jumapili kwamba mikutano hiyo ilikuwa haramu na imepigwa marufuku.
Maeneo mengine jijini Nairobi yalikuwa yametulia baada ya usalama kuimarishwa ya kutosha huku maafisa wa polisi wakionekana wakishika doria kila mahali.