Harmonize Kubadili Dini Hivi Karibuni?

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Christina Shusho kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu walichozungumza na Harmonize mwaka jana walipokutana ghafla nchini Kenya, Harmonize akamkimbilia na kumbusu miguu.
Katika mahojiano maalum na kituo kimoja cha habari nchini Tanzania, Shusho alisema baada ya kitendo hicho kunaswa walikwenda chumba cha faragha na kufanya mazungumzo makubwa zaidi.
Shusho alisema kuwa moja ya jambo ambalo alifurahi kusikia kutoka kwa msanii huyo ni kupenda kusikiliza muziki wake wa Injili.
“Nilipata nafasi ya kukaa na kuzungumza naye, alisema jambo ambalo lilinigusa moyo sana, alisema ‘Dada napenda sana nyimbo zako, ukiimba nyimbo zako unatuelimisha juu ya Mungu, unatuelekeza kumjua Mungu., unatuachia chaguo la kuamua kumfuata Mungu au kuendelea na mambo yetu,” Shusho alinukuu maneno hayo kutoka moyoni mwa Harmonize.
Alisema msanii huyo pia alimalizia kwa kumwambia kwa sauti ya dhati kuwa kutokana na hamasa anayoipata kwenye nyimbo zake ipo siku atamuona kanisani.
“Hilo linanifanya nisikilize nyimbo zako sana, navutiwa sana na kutaka kujua unachoimba. Na nina uhakika ipo siku utaniona kanisani,” Shusho alimnukuu Harmonize.
Inafahamika kuwa Harmonize ni Muislamu na Shusho ni Mkristo aliyeanzisha kanisa lake mwaka jana.
Kauli ya kwamba Harmonize siku moja atajiunga na kanisa hilo na Shusho ni ishara kwamba huenda anafikiria kubadili dini yake kutoka Uislamu na kwenda Ukristo.
Shusho alisema kuwa kauli ya Harmonize ilimpa moyo sana na alijua kuwa kuna watu wengi anaowagusa na kuwaweka karibu na Mungu kupitia uimbaji wake.