Feisal Salum Kuvunja Mkataba Na Yanga

Ni siku chache tu zimepita tangu Feisal Salum atenguliwe shauri lake na shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania ( TFF) na siku ya Jumatatu mchezaji huyo amewasili tena katika ofisi za shirikisho hilo akipeleka barua ya maombi ya kutaka kuvunja mkataba wake na timu ya Young Africans sports club.
Wakati alipokuwa akipeleka barua hiyo, Feisal aliwasili katika ofisi za TFF akiambatana na wakili wake wa sasa Jasmin Razack ambaye ni wakili mbobezi katika masuala yahusuyo stahiki za wachezaji wa mpira wa miguu.
Katika uwasilishwaji wa barua hiyo ya kuvunja mkataba, Jasmin ameeleza ya kuwa mkataba baina ya mchezaji na timu hauwezi kuvunjwa kutokana na kuwa TFF pekee ndiyo yenye mamlaka juu ya uvunjwaji wa mikataba baina ya pande hizo mbili.
Baada ya uwasilishwaji wa barua hiyo kwa TFF, wakili Jasmin amewataka wachezaji kutilia maanani mikataba wanayoisaini kwa kuipitia kwa uangalifu na kuwataka wachezaji kuchukua muda kusoma kanuni pamoja na kuzielewa kabla ya kutia saini katika mikataba yao.
Baada ya hayo yote kumalizika Jioni ya siku hiyo, klabu ya soka ya Yanga imetoa taarifa ikimtaka Feisal kuwasili katika kambi kwa ajili ya kuendelea na mazoezi na timu hiyo.
Pia Yanga imetoa nafasi kwa timu yoyote itakayomtaka mchezaji huyo kuingia katika mazungumzo na timu hiyo huku ikitoa nafasi kwa ajili ya wawakilishi wa Feisal kuongea na timu hiyo juu ya maboresho ya mkataba wa Feisal akiwa Yanga.