DCI Kuchunguza Helikopta Ya Mbunge David Pkosing
Helikopta ya Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing ambayo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Wilson imefanyiwa uchunguzi wa kina leo Jumamosi asubuhi na wapelelezi kutoka idara ya upelezi na makosa ya Jinai (DCI).
Kulingana na wakili wake Danstan Omari, uchambuzi huo ni sehemu ya uchunguzi wa madai ya mteja wake kuhusika katika ujambazi na utakatishaji fedha.
Chopa hiyo ilianza kuchunguzwa baada ya kutumika kuwasafirisha wanaume saba kutoka Mahakama ya Kitale baada ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ujambazi. Waliachiliwa kila mmoja kwa bondi ya Sh elfu 10,000, ambayo mbunge huyo anasema alilipa kama kiongozi wao.
Pkosing alikamatwa Alhamisi jioni na kupelekwa katika Makao Makuu ya DCI kwenye Barabara ya Kiambu. Inasemekana alikataa kurekodi maelezo bila kuwepo kwa mawakili wake na baadaye aliachiliwa saa 10:30 usiku.
Siku ya Ijumaa asubuhi alienda katika Makao Makuu ya DCI na kisha kuitwa jioni baadaye.
Akihutubia wanahabari, Pkosing alikanusha madai hayo akisema kuwa yeye ni Mkenya anayependa amani na hajawahi kunufaika na mapato yoyote ya wizi.
Kuhusu suala la chopa nyeupe ambayo inadaiwa kutumika kuwapa silaha majambazi hao, mbunge huyo alikanusha na mawakili wake akisema iwapo ndivyo ingekuwa hivyo, basi Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya ingelifanya hilo muda mrefu uliopita.
Kulingana na Pkosing, chopa yake ni nyeupe na kijani huku chopa inayodaiwa ikiwa nyeupe pekee bila rangi ya Kijani.
Mbunge huyo alijitetea kuwa anatajwa na wachunguzi akisema viongozi wengi walitoa maoni yao kuhusu suala la wizi wa ng’ombe, lakini ni yeye pekee aliyeitwa na kuhojiwa.