Home » Mwenyekiti Wa Baraza La Wazee LUO Willis Otondi Afariki Hospitalini

Mwenyekiti Wa Baraza La Wazee LUO Willis Otondi Afariki Hospitalini

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa jamii ya Luo  Willis Opiyo Otondi amefariki.

 

Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisumu Elisha Oraro amethibitisha kufariki kwa Mzee Otondi Ijumaa asubuhi.

 

Ker Otondi amekuwa akiingia na kutoka hospitalini miezi ya hivi majuzi na alilazwa hivi majuzi katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.

 

Spika Oraro amesema Mzee Otondi alifariki katika hospitali ya Avenue alikokuwa amehamishiwa.

 

Oraro anasema jamii ya Wajaluo wamempoteza mtu mkubwa ambaye licha ya umri wake, alijitahidi kuielekeza jamii katika mwelekeo sahihi kijamii, kisiasa na kiuchumi.

 

Jumapili wiki jana, kiongozi wa Azimio Raila Odinga na viongozi wengine wengi walimtembelea Otondi anayeugua katika JOOTRH.

 

Otondi amekuwa kwenye usukani wa Baraza hilo tangu kufariki kwa aliyekuwa Ker wakati huo marehemu Riaga Ogallo.

 

Hata hivyo, kumekuwa na mrengo wa wazee unaoongozwa na Nyandiko Ongadi ambaye pia anadai uenyekiti wa baraza mwavuli la wazee katika jamii ya Waluo.

 

Mzee Otondi anatoka eneo la Nyahera katika kaunti ndogo ya Kisumu Magharibi.

 

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amemomboleza Mzee Otondi kama nguzo ya umoja wa jamii akisema alihudumu kwa adabu na kujitolea.

 

“Kwa niaba yangu binafsi, familia yangu, chama chetu na taifa zima la Wajaluo, natuma risala za rambirambi kwa familia ya Bw. Otondi na ndugu wengine wote aliohudumu wakati wa utawala wake kama Ker.

 

“Mzee Otondi alikuwa nguzo ya umoja wa jamii na alihudumu kwa adabu na kujitolea. Inasikitisha kumpoteza katika hatua hii maalum ya maisha ya jamii,” alisema Odinga.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!