Serikali Yaomba Wakenya Kutoa Msaada Wa chakula Kusaidia Uturuki
Huku shughuli za uokoaji zikiendelea kule Uturuki na Syria baada ya tetemko lilitokea jumatatatu na kuwauwa maelfu ya watu, sasa Serikali ya Kenya imetoa wito kwa Wakenya wenye moyo kutoa msaada wa vyakula na vitu vingine vya msaada ili kusaidia waathirika.
Kulingana na Waziri wa masuala ya kigeni Alfred Mutua, ametoa risala zake kwa mataifa hayo huku shughuli za uokoaji zikiingia siku yake ya tatu hii leo Jumatano.
Aidha taarifa kutoka kwa baadhi ya mataifa yanaripoti kuwa takribani watu elfu nane wamepatikana wamefariki katika mkasa huo kwa kunaswa ndani ya vifusi vya majumba yaliyoporomoka usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya zilizala ya kiwango cha juu kuzuka.
Mutua ameonesha kuguswa kwake na kile kilichotokea huku akisema kuwa Kenya na Uturuki wanashiriki matukio sawa ambayo yametokea kipindi ambapo janga la korona limepungua.
Waziri Mutua amesema kuwa hivi karibuni watatoa taarifa Zaidi jinsi Wakenya wa kutoa msaada wataweza kufanya hivyo ili msaada huo uweze kuwafikia walioathirika na zilizala Uturuki kwa haraka.
Katika taarifa hiyo, waziri huyo amesisitiza taarifa ya katibu wa masuala ya wanaoishi nje ya nchi kwamba mpaka sasa hakuna Mkenya aliyeripotiwa kuathirika au kufariki katika mkasa huo ambao jamii ya kimataifa imejitoa kwa hali na mali kutoa msaada na kuokoa kufukua vifusi hivyo kwa haraka.