Home » Serikali Yaanza Mchakato Wa Kumsaka Msemaji Wa Serikali

Serikali Yaanza Mchakato Wa Kumsaka Msemaji Wa Serikali

Serikali  kupitia Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) imeanza mchakato wa kujaza nafasi ya aliyekuwa Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna.
Tangazo hilo limetolewa kupitia notisi ya umma ya leo Jumanne, Februari 7.

 

Kulingana na PSC, msemaji huyo atapokea mshahara wa kila mwezi wa shilingi 970,000 ikijumuisha mshahara wa kimsingi kati ya shilingi 292,000 na shilingi  576,000.

 

Malipo hayo yanakuja kutokana na marupurupu ya nyumba, ya burudani, , ya watumishi wa ndani, ya likizo na malipo ya matibabu yote yanafikia zaidi ya shilingi  400,000.

 

Waombaji wa nafasi hiyo lazima wawe na uraia wa Kenya na wanapaswa kuwa wamefanya kazi kwa muda usiopungua miaka 15 kama mtaalamu wa vyombo vya habari au mawasiliano.

 

Shahada ya kwanza katika fani zinazohusiana na vyombo vya habari (media) kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa pia ni lazima.
Msemaji atawasilisha sera, programu, na mipango ya serikali kwa umma kupitia njia za vyombo vya habari.

Jinsi ya kutuma maombi ya kazi hii

Watu walio na nia na sifa stahiki wameshauriwa kutuma maombi yao mtandaoni kupitia tovuti ya tume www.publicservice.go.ke. kabla ya tarehe 27 Februari 2023.

Atakayefaulu atachukua nafasi ya Oguna ambaye alikuwa mmoja wa maafisa wakuu wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na kuchukua wadhifa huo Mei 7, 2019, kutoka kwa Eric Kiraithe.

 

Oguna alikuja kujulikana kutokana na jukumu lake kama msimamizi wa Ofisi ya Masuala ya Umma ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na Msemaji wa KDF mwanzoni mwa Operesheni Linda Nchi, wadhifa alioshikilia kati ya 2011-2013.

 

Alichangia pakubwa katika kuwapa Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya (KDF) taswira ya umma kwa kuwafahamisha Wakenya kuhusu maendeleo ya vita nchini Somalia.

 

Mnamo Oktoba 2022, Oguna aliacha wadhifa huo baada ya kuteuliwa na Gavana wa Siaya James Orengo kuhudumu kama Mkuu wake wa Majeshi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!