Home » Azimio Yalinganisha Mikutano Yake Ya Hadhara Na Ule Uliotimua Issack Hassan Afisini

Azimio Yalinganisha Mikutano Yake Ya Hadhara Na Ule Uliotimua Issack Hassan Afisini

Muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One-Kenya ukiongozwa na Raila Odinga, unapanga mikutano ya hadhara inayolenga kujadili masuala mazito yanayoiathiri Kenya, huku Tume ya Uwiano na Utangamano ikimtaka kiongozi huyo kusitisha mikutano hiyo kwa hoja kwamba italiyumbisha taifa linalojaribu kusimama tena baada ya uchaguzi mkuu ulioshuhudia ushindani mkali.

 

Katika kipindi cha majuma mawili, Raila ameandaa mikutano miwili ya hadhara jijini Nairobi, na wafuasi wake wanasema kuwa ndio mwanzo wa ngoma…Mikutano hiyo ikilenga kuishinikiza serikali ya rais William Ruto kuleta mageuzi pamoja na kupunguza gharama za maisha ambazo zimepanda si haba.

 

Ikumbukwe kwa sasa bei ya gesi imepanda kutoka shilingi elfu 1200 hadi shilingi elfu 1500.

 

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, kiongozi wa wachache kwenye bunge la taifa Opiyo Wandayi, amesema kuwa Azimio la Umoja litaanda mkutano mwingine katika mtaa wa Kibra leo hii jumapili ambao ni ngome ya siasa ya Raila, punde tu kiongozi huyo wa upinzani atakaporejea nchini kutoka Afrika Magharibi.

 

Juma moja baadaye, mkutano mwingine wa hadahara utafanyika katika kaunti ya Machakos, huku wafuasi wao wakitakiwa kufika kwa wingi na kwa utele.

 

 

Tangu kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka uliopita, Raila ameyapinga matokeo hayo, licha ya mahakama ya Juu zaidi nchini kuthibitisha ushindi wa Ruto.

 

Ikumbukwe kuwa Rais Ruto amekamilisha miezi mitatu tu, tangu achaguliwe kuwa rais.

 

Upinzani unasema kuwa mikutano hiyo ya hadhara, itakuwa sawa na ile iliyoandaliwa mwaka 2016, iliiyochangia kutimuliwa kwa mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC wakati huo Issack Hassan.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!