Home » Wanaharakati: Mpango Wa Kitambulisho Cha Kidijitali Kugharimu Wakenya

Wanaharakati: Mpango Wa Kitambulisho Cha Kidijitali Kugharimu Wakenya

Mashirika ya kiraia chini ya mwavuli wa Operesheni Linda Ugatuzi yameeleza nia yao ya kuwasilisha ombi mahakamani la kuzuia kuanzishwa kwa Kitambulisho kipya cha Kibinafsi (UPI).

 

Wakiongozwa na mwanaharakati na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Fred Ogola, timu hiyo imesema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo ni ufujaji wa rasilimali za umma kwani ulikuwa mradi sawa na kadi ya Huduma Namba, uliotekelezwa na utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na ukaishia kutofanya kazi.

 

Zaidi ya hayo, wameteta kuwa maelfu ya Wakenya waliopewa kandarasi ya kusambaza Huduma Namba watapoteza pesa na kazi.
Ogola amedai kuwa serikali ilinuia kuwapa kandarasi raia wa Pakistan ili kusambaza vitambulisho hivyo badala ya kuwapa kandarasi wataalamu wa Kenya.

 

Wakati huo huo, amekariri kuwa Wakenya tayari wanahangaika na gharama ya juu ya maisha na mabilioni yatakayotumika kusambaza kitambulisho kipya cha kidijitali yataathiri uchumi wa Kenya.

 

Tofauti pekee kati ya UPI na Nambari ya Huduma kulingana na wanaharakati, ilikuwa jina na kiasi cha mabilioni ambacho kitatumika katika kufanikisha hati iliyopendekezwa.

 

Mnamo Februari 2023, waziri wa mawasiliano na teknolojia Eliud Owalo alitangaza kwamba serikali itakamilisha usambazaji wa vitambulisho vya kidijitali kufikia Februari 2024.

 

Alibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa huduma kama vile afya, usalama wa taifa na ukusanyaji wa kodi.

 

Mapema Mei 24, Rais William Ruto alimpa Colin Howell, mbunifu anayetambulika kimataifa, kazi katika utengenezaji wa vitambulisho vya kidijitali, baada ya kumvutia kwa uwasilishaji wa Power-Point kuhusu jinsi safari yake barani Afrika ilivyochochea kubuniwa kwa pasipoti ya Kenya.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!