Home » Kaunti Ya Siaya Yaripoti Visa 120 Vya Kipindupindu Kufikia Sasa

Kaunti Ya Siaya Yaripoti Visa 120 Vya Kipindupindu Kufikia Sasa

Visa vya ugonjwa wa kipindupindu vilivyoripotiwa Siaya vimefikia 120, huku gavana James Orengo na kamishna wa kaunti hiyo Jim Njoka wakiwataka wakaazi kuunga mkono juhudi za kudhibiti ugonjwa huo hatari kwa kuzingatia usafi.

 

Wakizungumza maeneo tofauti, Orengo na Njoka walilalamika kuwa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza katika kaunti hiyo miezi miwili iliyopita bado hazijazaa matunda, huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka polepole.

 

Orengo, ambaye alizungumza wakati wa kuzindua ambulansi za kisasa katika makao makuu ya kaunti hiyo alisema kuwa timu ya matabibu kutoka serikali ya kaunti imekita kambi katika ufuo wa Rarieda na kaunti ndogo za Bondo ambazo ndizo viini vya ugonjwa huo.

 

Alisema kuwa serikali yake ina dawa za kutosha kukabiliana na ugonjwa huo na kuwataka wananchi kumkimbiza katika kituo cha afya kilicho karibu na yeyote atakayeonyesha dalili za kuharisha na kutapika.

 

Naye kamishna wa kaunti Jim Njoka ambaye alihutubia pubic wakati wa maadhimisho ya siku ya Madaraka mwaka huu katika uwanja wa KMTC katika mji wa Siaya alipongeza serikali ya kaunti kwa hatua yake ya haraka ya kudhibiti kuenea kwa kipindupindu.

 

Njoka hata hivyo alitoa wito kwa idara ya afya ya serikali ya kaunti kuendeleza msako dhidi ya mikahawa ambayo haizingatii matakwa ya afya ya umma.

 

Msimamizi huyo aliwataka wakazi wa Siaya kujiunga na vita dhidi ya kuenea kwa ugonjwa huo kwa kuhakikisha kuwa mazingira yao ni safi na yanazingatia usafi wa kimsingi.

 

Viongozi hao walifafanua kuwa hadi sasa, ni vifo vinne pekee vilivyoripotiwa katika kaunti hiyo na kwamba vifo vyote vilitokea katika hospitali ndogo ya rufaa ya kaunti ya Bondo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!