Home » Waziri Kindiki Arekebisha Muda Wa Kusubiri Pasipoti

Waziri Kindiki Arekebisha Muda Wa Kusubiri Pasipoti

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametangaza kwamba Wakenya walio na dharura watashughulikiwa ndani ya saa 24.

 

Akiwahutubia wanahabari kutoka Harambee House katika Kaunti ya Nairobi, Kindiki ameeleza kuwa ratiba ya saa 24 itatumika kwa wale walio na dharura za matibabu na elimu.

 

Waziri huyo amebainisha kuwa ratiba hiyo itatekelezwa kuanzia wiki ya mwisho ya Juni 2023 baada ya Idara ya Uhamiaji kuondoa kasoro iliyokuwepo.

 

Kwa upande mwingine, ameshikilia kuwa waombaji wengine watapata stakabadhi zao za kusafiri ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya kutuma maombi.

 

Waziri huyo ameeleza kuwa mabadiliko hayo yatasaidia serikali kushughulikia maswala ya waombaji pasipoti ambao walikuwa wakisubiri kwa miezi kadhaa kupata stakabadhi hizo.

 

Amefichua kuwa mrundikano wa stakabadi za kusafiria 42,000 ulisababishwa na kuharibika kwa printa iliyotumika kubinafsisha hati za kusafiri.

 

Kindiki ameongeza kuwa wanajitahidi kushughulikia ucheleweshaji huo katika siku saba zijazo.

 

Katika kuhakikisha utendakazi mzuri wa zoezi hilo, Waziri Mkuu amedai kuwa atasimamia shughuli hiyo binafsi ili kuhakikisha muda unatekelezwa.

 

Zaidi ya hayo, ametangaza kuwa watachukua mabadiliko ya kiutawala katika idara hiyo kufuatia malalamishi ya Wakenya kuhusu kutaka hongo na maafisa wa idara hiyo.

 

Waziri huyo ameongeza kuwa alikuwa ametuma baadhi ya wafanyakazi wake kwenye misheni ya kutafuta ukweli katika idara na kufichua utovu wa nidhamu wa baadhi ya maafisa.

About The Author

error: Content is protected !!