Serikali Yakosoa Wanakandarasi Katika Marekebisho Mapya

Bodi ya Wahandisi ya Kenya, kwa ushirikiano na washikadau wengine wa serikali, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Uchukuzi, imeanzisha mageuzi katika sekta ya ujenzi.
Katika hatua za hivi punde zaidi, Bodi ya Wahandisi ya Kenya ilizindua tovuti ya mtandaoni inayolenga wajenzi wanaotekeleza miradi mbalimbali.
Kulingana na bodi, wahandisi wote walioidhinishwa lazima wajiandikishe kwenye tovuti ya mtandaoni. Kando na kupakia sifa zao zote, wahandisi na wajenzi wa mradi lazima wajumuishe miradi yote wanayofanya.
Tovuti hiyo itafuatilia miradi yote ili kushughulikia suala la majengo kubomoka na ubovu wa ujenzi wa barabara.
Wizara ya Uchukuzi, kwa upande wake, imepongeza mpango huo ikionyesha kuwa ulikuwa muhimu katika kushughulikia matukio kadhaa ya ubovu wa miradi ya barabara ambayo iliilazimu serikali kuwasimamisha kazi baadhi ya wanakandarasi.
Katibu Mkuu wa Barabara Joseph Mbugua amesisitiza kuwa tovuti hiyo itaboresha utoaji wa huduma na kuharakisha miradi mbalimbali nchini ili kuepuka ufujaji wa rasilimali za umma.
Mnamo Ijumaa, Mei 14, Rais William Ruto alimfukuza mwanakandarasi mmoja kutoka mradi wa maji wa Ksh500 bilioni katika Kaunti ya Machakos.
Uongozi wake ulilazimika kumfukuza mkandarasi kabla ya mradi kukamilika baada ya kufeli kufanya kazi ilivostahili .