Home » Kifungo Cha Mwanaume Wa Italia Aliyenajisi Mtoto Kisumu Chapunguzwa

Kifungo Cha Mwanaume Wa Italia Aliyenajisi Mtoto Kisumu Chapunguzwa

Mahakama kuu mjini Kisumu imekubali hukumu ya Mahakama ya Winam dhidi ya rufaa ya raia wa Italia Paolo Camelini, ambaye alifikishwa mahakamani kwa kumnajisi mtoto wa miaka 3 katika mtaa wa Manyatta huko Kisumu Februari 2022.

 

Raia huyo wa Italia alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mtoto huyo lakini akakata rufaa kwa msingi kwamba mahakama ya chini ilifanya makosa kisheria kwa kuruhusu mpatanishi kutoa ushahidi kwa niaba ya mwathiriwa.

 

Pia alihimiza kwamba mahakama hiyo ilishindwa kutambua kwamba ushahidi wa mdomo wa mpatanishi haukuwa wa mwathiriwa na kwamba matumizi ya mara kwa mara ya jina ‘Paolo’ na mwathiriwa hayakuwa ushahidi wa kutosha kumtambua mtu yule.

 

Hata hivyo, Jaji Roseline Aburili amekubaliana na mahakama ya chini kwamba mwathiriwa, akiwa ni mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 3, hawezi kutoa ushahidi, hivyo haja ya mpatanishi kutoa ushahidi kwa niaba ya mwathiriwa na kwamba ushahidi uliotolewa na mpatanishi ni wa mwathirika.

 

Mahakama imesema zaidi kwamba upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili Mkuu Mashtaka John Okoth, ulithibitisha ushahidi wa unajisi na utambulisho wa jamaa Yule mwitaliano pamoja na umri wa mwathiriwa bila shaka yoyote.

 

Mahakama, hata hivyo, ilitupilia mbali kifungo cha maisha ambacho kilikuwa kimetolewa na mahakama ya chini na kubadilisha kifungo hicho hadi miaka 30, ikisema mahakama ya chini haikuzingatia ukweli kwamba jamaa yule alikuwa mkosaji wa kwanza.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!