Home » Maseneta Kufanya Vikao Turkana

Bunge la Seneti litafanya vikao vyake vilivyopewa jina la Seneti Mashinani katika Kaunti ya Turkana mnamo Septemba kuanzia tarehe 25 hadi 29, 2023.

 

Maseneta hao Jumanne hii leo watajadiliana kuhusu hoja ya Kiongozi wa Wengi katika Seneti kuwasilisha azimio la Kamati ya Biashara ya Seneti ambayo ilikubaliana Kaunti ya Turkana kama Kaunti mwenyeji.

 

Kulingana na Kamati ya Seneti ya Biashara, vikao hivyo vinakusudiwa kutoa mwingiliano kati ya ngazi ya Kitaifa na Kaunti ya serikali na kuimarisha mwingiliano kati ya Seneti na serikali za kaunti kama njia ya kuleta Seneti karibu na kaunti na umma kwa jumla.

 

Maseneta hao walibaini kuwa kuna mafanikio kadhaa ambayo yamepatikana kutokana na kufanya vikao nje ya Nairobi.

 

Vikao vya awali vilifanyika katika Kaunti za Uasin Gishu na Kitui mnamo Septemba, 2018 na Septemba, 2019, mtawalia.

 

Seneti ya Mashinani haikufanyika mnamo 2020 na 2021 kwa sababu ya janga la korona.

 

Uamuzi wa Kamati ya Biashara ya Seneti unafuatia azimio lililofuata la Seneti lililotolewa tarehe 8 Machi, 2023, kufanya vikao na kamati katika kaunti kwa muda wa wiki moja ndani ya mwezi wa Septemba katika kila Kikao cha 4 cha Seneti, isipokuwa wakati wa mwaka wa uchaguzi.

 

Malengo ya vikao hivyo miongoni mwa mengine ni kukuza jukumu na kazi ya Seneti na kuongeza ufahamu wa umma kuhusu Biashara ya Seneti na Bunge kwa ujumla, kuangazia fursa zilizopo na mpya za kushiriki katika mchakato wa kutunga sheria kando na kuendeleza na kuimarisha ushirikiano katika ngazi ya serikali ya kaunti.

 

Mnamo Aprili 2023, afisi ya Karani wa Seneti ilifanya uchunguzi katika Kaunti za Marsabit, Mandera, Isiolo, Turkana, Kisii, Busia, Laikipia, Nyamira na Taita Taveta kisha kuwasilisha ripoti za kila Kaunti kwa Kamati ya Bunge la Seneti ili kuzingatiwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!