Waziri Kindiki Awaonya Maafisa Wa Polisi
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametoa onyo kali dhidi ya maafisa wa polisi ambao watapatikana wakiwahangaisha wafanyabiashara katika msako haramu wa pombe katika eneo la bonde la ufa.
Akizungumza wakati wa kongamano la kudhibiti utumizi wa dawa za kulevya mjini Nakuru hii Jumatatu, Waziri Kindiki ameonya kuwa maafisa waliopewa jukumu la zoezi hilo hawafai kuwahangaisha wafanyabiashara walio na leseni.
Ameonya kuwa hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika kukiuka agizo hilo.
Waziri wa Mambo ya Ndani pia amesema kuwa tayari amepokea ripoti za unyanyasaji kwa wafanyabiashara walio na leseni, akiwataka maafisa kufanya kazi kwa uangalifu kulingana na miongozo iliyotolewa.
Kindiki ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye amekuwa akipigania vita vya biashara haramu ya pombe nchini.
Gachagua katika hotuba zake zilizopita amewaagiza wasimamizi wa kaunti kuchukua mkondo wa kukabiliana na utumizi mbaya wa dawa za kulevya na pombe katika maeneo yao.
Vile vile ametishia kuchukua hatua kali za serikali kwa wasimamizi wa kaunti watakaopatikana wakiwasaidia walanguzi wa dawa za kulevya kote nchini.