Uhuru Amwonya Ruto
Kwa mara ya kwanza hii leo Jumamosi, Mei 27 Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa onyo lililoelekezwa kwa Rais William Ruto kuhusu kuporomoka kwa mazungumzo ya pande mbili.
Katika mkutadha wa “Kukuza Demokrasia kwa Maendeleo na Utangamano,” katika mkutano wa Kuapishwa kwa Rais wa 2023 uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano huko Abuja Nigeria, Uhuru ameonyesha kuwa alikuwa akishinikiza mazungumzo ya kukuza umoja nchini Kenya.
Kwa hivyo ameonya utawala wa Kenya kwanza dhidi ya kutetea fikra za kujijali pekee, akisema kwamba itasababisha mgawanyiko wa nchi.
Aidha, Uhuru ametoa maoni kwamba kupuuza mazungumzo na mgawanyiko wa upinzani, unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kutaathiri vibaya mkakati wa ajenda ya maendeleo ya taifa.
Rais huyo wa zamani amewaambia wajumbe kuwa kushirikisha upinzani ilikuwa muhimu katika kukuzamaendeleo na uchumi.
“Ninasalia kwa ukweli kwamba lazima niendelee kushiriki katika kukuza amani katika nchi yangu ya Kenya. Ninatumia sauti yangu na jukwaa kuwashawishi, haswa walio madarakani, kwamba mazungumzo na wale wanaopinga ushindi wao sio udhaifu wala si kunyimwa ushindi wao bali ni chombo kinachohitajika sana kwa ajili ya kuunda Kenya iliyojumuishwa zaidi ambayo inaweka mwelekeo wa maendeleo mbele.
“Njia ambayo inakidhi mahitaji ya wote katika jamii yetu. Na ninawakumbusha kuwa mawazo ya mshindi huchukua yote yanaweza tu kusababisha mgawanyiko na kudumaza ajenda yetu ya maendeleo ya kitaifa,” Uhuru alisema.
Hivyo amemshauri Rais mteule wa Nigeria, Bola Tinubu, kuhakikisha utawala wake unajenga taifa lenye ustawi na umoja. Ijapokuwa Tinubu hakuwepo katika ukumbi huo, Uhuru amesisitiza kwamba lazima aongoze taifa lililoungana bila kujali kama walimuunga mkono au la wakati wa shughuli ya uchaguzi.
Maoni yake yamekuja baada ya timu ya Azimio kusimamisha mazungumzo ya pande mbili ikishutumu upande wa Kenya Kwanza kwa kukosa kutimiza matakwa yao.
Azimio baadaye ilikataa mwaliko kutoka Kenya Kwanza wa kurejelea mazungumzo Ijumaa, Mei 26.
Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, akiongoza upande wa Azimio, alidokeza kuwa wataheshimu tu mwaliko huo ikiwa Kenya Kwanza itakubali matakwa yao.
Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa na Azimio ni pamoja na hakikisho kwamba Kenya Kwanza itajitolea kupunguza gharama ya maisha, kuangazia sava za uchaguzi, na kusimamisha uundaji upya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hata hivyo, upande wa Kenya Kwanza ulieleza kujitolea kwao kushirikisha Azimio wakati wowote watakapoitisha mkutano kushughulikia maswala yao.