Serikali Kuongeza Bajeti Ya Chakula Cha Shule
Katibu Mkuu Idara ya Elimu ya Msingi, Dkt. Belio Kipsang, ametangaza kuwa Serikali ya Kitaifa, katika Mwaka ujao wa Fedha wa 2023/2024, itafadhili mara mbili mpango wa chakula shuleni kutoka Ksh 2 bilioni hadi bilioni 4 na kufanya kazi kwa karibu na Serikali za Kaunti ili kuongeza ulishaji na uhifadhi wa watoto shuleni.
AMEonyesha kuwa chakula na lishe vina jukumu muhimu sana katika ustawi wa wanafunzi katika suala la ukuzaji wa uwezo wao wa kiakili.
Katibu huyo mkuu alikuwa akizungumza alipoongoza uzinduzi wa Mpango wa Maziwa Shuleni katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Amedokeza kuwa wito wa jumla wa mpango wa lishe shuleni ni kuunga mkono serikali kufikia elimu ya msingi kwa wote na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo yanaambatana na Mkataba wa Elimu wa serikali ya Kenya Kwanza.
Kipsang amebainisha kuwa mpango wa chakula shuleni, umekuwa mkakati muhimu wa kuwafikia watu waliotengwa na wanaoishi katika mazingira magumu na wale walio katika lindi la umaskini mijini.
Dkt Kipsang amesema kuwa ni jukumu la pamoja kushirikiana katika ngazi zote za serikali, kuhakikisha kwamba watoto wana uwezo wa kuwa shuleni huku akisisitiza dhamira na azma ya serikali ya kutoa maziwa ya shule katika maeneo yote ya uakme ASAL, na maeneo ya makazi ya watoto wenye mahitaji maalum.
Vile viel ametoa wito kwa magavana katika kaunti zote 47 kuunga mkono mpango huo, ambao ni mafanikio kwa sekta ya kilimo na elimu, akibainisha kuwa ni muhimu kwa kuongeza uandikishaji, kuleta utulivu wa mahudhurio ya mwanafunzi shuleni, kuongeza usawa wa kijinsia kwa sababu watoto wa jinsia zote watakuwa shuleni na kuboresha mabadiliko na wakati uo huo kuchangia kuboresha sekta ya afya na lishe kwa watoto.
Kwa upande wa kilimo, itaunganisha chakula cha shule na uzalishaji wa ndani wa kilimo, pia itaongeza upatikanaji wa wakulima wadogo kwenye soko la chakula shuleni lililopo.
Hata hivyo amepongeza hatua ya Uongozi wa Kaunti ya kutoa maziwa ya shule kwa shule za ECDE katika Kaunti hiyo, ambayo amesema, itaongeza uhifadhi, mpito na kuhakikisha kuna mafanikio katika upatikanaji wa elimu bora.