Wabunge Wapendekeza Nyongeza Ya Ksh 7.4B Kwa Sekta Ya Kilimo
Kamati ya Bunge ya Kilimo na Mifugo inataka mgao wa bajeti ya kilimo kwa mwaka ujao wa kifedha uongezwe kwa Ksh 7.4 bilioni hadi Ksh 71.8 bilioni.
Mgao huo wa ziada unatarajiwa kufadhili mpango wa ruzuku ya mbolea, kulipa wasagaji kwa ruzuku ya unga wa mahindi ya mwaka jana na pia kuwalipa wakulima walioshiriki katika mpango huo.
Kamati ya Bunge ya Kilimo na Mifugo imebainisha kuwa kati ya hatua tisa ya thamani itakayobadilisha Ajenda Bottom up economi-model, sita iko chini ya Wizara ya Kilimo na Mifugo.
Wabunge wamependekeza Ksh 4 bilioni ziongezwe kwa pendekezo la Ksh 4.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mpango wa ruzuku ya mbolea katika mwaka ujao wa kifedha.
Wabunge hao wameteta kuwa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea unahitaji Ksh 13.5 bilioni za kutosha ili kutoa mbolea ya ruzuku kote nchini.
Kamati hiyo pia imependekeza nyongeza ya Ksh 1 bilioni kwa ajili ya kulipia deni la wakulima walioshiriki katika mpango wa kuuza mifugo.