Wabunge Waasi Wa Jubilee Wapuuzilia Kutimuliwa Kwao
Wabunge waasi wa Jubilee wakiongozwa na mbunge wa EALA Kanini Kega wamepuuzilia mbali hatua ya chama hicho kuwatimua wakidai kuwa ni batili.
Katika mazungumzo, Kega ameapa kukipigania chama hicho kutoka kwa mrengo wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.
Walisema wataandaa Kongamano tofauti la Wajumbe wa Kitaifa mnamo Julai ili kuweka muhuri mamlaka yao na kufanya mabadiliko zaidi.
Mbunge mteule Sabina Chege na Kanini Kega walishirikiana na baadhi ya wabunge waliochaguliwa na Jubilee kumtimua aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kutoka kwa uongozi wa chama na kumtaja Sabina Chege kuwa kiongozi mpya wa chama na Kanini Kega kuwa Katibu Mkuu mpya akichukua nafasi ya Jeremiah Kioni.
Mahakama ya mizozo ya vyama vya siasa bado haijaamua kiongozi halali wa chama ni nani baada ya msajili wa vyama vya siasa kurudisha mzozo huo kwenye mahakama hiyo.
“Inasikitisha kwamba Rais wa zamani amechagua kuwa katika upande mbaya wa historia kwa kukaidi uamuzi halali wa chama na zaidi aliacha kuwa kiongozi wa chama mnamo Machi 14, 2023 kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Mafao ya Wastaafu wa Rais.kwa sasa hana mamlaka ya kuitisha au kuongoza mkutano wowote wa chama, adhabu hiyo haikubaliki na ni kinyume cha sheria na inatia doa ofisi, chama hakitasita kumchukulia hatua kiongozi huyo wa zamani wa chama.”