Raila Awataka Viongozi Kuheshimu Uhuru
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amejitetea na kulaani mashambulizi ya hivi majuzi ya kisiasa dhidi ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Akizungumza hii leo Jumatatu wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Chama cha Jubilee (NDC), Odinga ametaja mashambulizi hayo kuwa “ya kale na yasiyostahili.”
Kiongozi huyo wa upinzani amebainisha kuwa rais huyo mstaafu anafaa kutendewa kwa heshima na adabu.
Kwa upande wake, Kenyatta alisema hatababaishwa na baadhi ya viongozi aliowatuhumu kwa kutomheshimu.
Akizungumza katika Kongamano la (NDC) katika uwanja wa Ngong Racecourse jijini Nairobi, Kenyatta alisema alikuwa tayari kustaafu siasa kali baada ya kumpa mamlaka Rais William Ruto mwaka jana hadi baadhi ya watu ambao hawakutajwa majina walipoanza kumtisha.
Kenyatta amewashutumu wapinzani wake kwa kumdhulumu na hata akagusia shambulio la Machi kwenye shamba la familia yake Northlands huko Kiambu, akisema anasalia kuwa kiongozi wa Jubilee hadi wanachama wa chama hicho waamue kuchagua bosi mwingine.