Kisii: DCI Yanasa Sukari “Gushi”
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) mjini Kisii pamoja na polisi wameteketeza sukari iliyopakiwa upya kinyume na sheria katika jengo la ghorofa huko Magena, Kaunti ya Kisii.
Katika operesheni kali iliyotokana na taarifa kutoka kwa wananchi, OCPD wa eneo hilo Charles Opondo amethibitisha kukamatwa kwa mwanamke wa makamo, anayedaiwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu katika eneo hilo.
Watu hao hupakia tena sukari kutoka Tanzania na Uganda kwenye magunia yaliyoandikwa Mara, Sony na viwanda vingine vya kusaga sukari nchini.
Wakati wa msako huo wa Jumatatu asubuhi, washukiwa hao walipatikana wakiendesha shughuli zao katika mazingira machafu bila mashine za kupimia uzito.
Opondo alisema tayari wamefahamisha Shirika la Viwango la Kenya (KEBS) na maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) kwa uchunguzi kabla ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara sukari hiyo.
Mmiliki wa eneo hilo, Dorcas Kemunto anasema kwamba alikodisha nyumba hiyo kwa mtu mmoja kwa jina Sam Ouko ambaye bado yuko mafichoni, bila kujua kinachoendelea ndani ya nyumba hiyo.
Maafisa wa DCI wameanzisha msako wa kuwasaka watu wanaoaminika kuhusika na biashara ya sukari isiyoidhinishwa katika maeneo ya Mogonga, Kenyenya, Ogembo na pia Kisii.
Haya yanajiri huku serikali ikiendelea na msako wa kitaifa wa sukari ya magendo inayodaiwa kuingizwa nchini kinyume cha sheria.