Nelson Koech: Hakutakuwa Na ‘Handshake’

Mbunge wa Belgut Nelson Koech amesema kuwa maonyesho ya hadharani ambayo Rais William Ruto amefanya na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga katika siku chache zilizopita hayafai kuashiria kuwa kutakuwa na HANDSHAKE.
Hii ni baada ya wawili hao kushiriki jukwaa wakati wa mazishi ya Mukami Kimathi katika kaunti ya Nyandarua mnamo Jumamosi na kisha kuhudhuria fainali za Kip Keino Classic katika uwanja wa Kasarani.
Wawili hao baadaye walipamba mechi kati ya Gor Mahia na AFC Leopards uwanjani Nyayo jana Jumapili hali ambayo wakenya wameshabikia mitandaoni wengi wakisema ni wakati sasa wa handisheki.
Akizungumza kwenye kipindi cha runinga moja humu nchini, Mbunge Koech ameeleza kuwa matukio hayo hayafai kusingizia kuwa kuna kitu kinaendelea kati ya wawili hao, akiteta kuwa Rais Ruto amekuwa akisisitiza kwamba hakuna uwezekano wa kupeana mkono kati ya serikali na upinzani.
Kwa hivyo, mbunge huyo, amewataka Wakenya kupunguza matarajio yao na wasitafsiri vibaya mwingiliano wa wawili hao.
Iwapo kutakuwa na mijadala yoyote, Mbunge Koech ameongeza, hawawezi kuishia katika kupeana mkono na badala yake kutoa suluhisho la kukomesha maandamano dhidi ya serikali.
Aidha, haya yanatokana na madai ya Rais Ruto kwamba nia yake ya kufanya mazungumzo na Odinga inatokana kikamilifu na kutatua masuala ambayo yalisababisha ghasia na maandamano ya kuipinga serikali yaliyoongozwa na muungano wa upinzani wa Azimio.