Huenda El Nino Ikarejea Juni 2023
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya kwamba huenda mvua ya El Nino ikarejea mwaka 2023 kufuatia awamu ya miaka mitatu ya mvua aina ya La Nina.
El Nino ina sifa ya ongezeko la joto ya juu ya wastani wa bahari katika Bahari ya Pasifiki ya kitropiki ya kati na mashariki, na katika kipindi hiki upepo wa mashariki unaovuma huwa chini kuliko kawaida.
La Niña kwa upande mwingine inahusisha kupoeza kwa hali-joto ya bahari katika Pasifiki ya mashariki-kati ya ikweta, na pepo za mashariki zina nguvu zaidi.
El Nino hutokea kila baada ya miaka 3 hadi 5 na kusababisha mvua nyingi na mafuriko katika eneo la Afrika Mashariki.
FAO inasema hali hiyo inatabiriwa kurejea mwezi Juni 2023, huku hali ya ukame ikitarajiwa katika maeneo muhimu ya upandaji mazao ya marekani ya Kati, Kusini mwa Afrika na Asia ya Mashariki.
Ulimwengu ulipata tukio la tatu mfululizo la La Nina mnamo 2022 na mapema 2023, tukio nadra ambalo limetokea mara mbili tu tangu 1950.
Matukio ya La Nina kwa kawaida huhusishwa na hali ya mvua nchini Australia na hali ya ukame katika Marekani na Afrika Mashariki.
Katika Afrika Mashariki, athari za uzalishaji wa nafaka zilikuwa mbaya sana, huku nchi kadhaa zikipitia misimu mingi ya mazao ambayo hayakufaulu ambayo yalisababisha tahadhari za njaa nchini Somalia katika nusu ya kwanza ya 2022.
FAO inasema tukio la La Nina la 2023 lilimalizika rasmi Machi 2023.
Katika mwezi uliopita, kumekuwa na mvua kubwa iliyorekodiwa katika maeneo mengi ya nchi, huku Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya wiki jana ikitabiri kuwa mvua itaendelea kunyesha katika maeneo mengi.
Baadhi ya maeneo ya nchi yameshuhudia uharibifu wa miundo msingi, kama vile Barabara kuu ya Mai Mahiu-Narok iliyofungwa wiki jana karibu na mji wa Mai Mahiu baada ya nyufa kubwa kuibuka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.
Sehemu ya reli ya Kisumu-Nairobi eneo la Kobigori kaunti ya Kisumu pia imeharibiwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.