Home » Gavana Lusaka Achaguliwa Kuongoza Mazungumzo Ya Pande Mbili

Gavana Lusaka Achaguliwa Kuongoza Mazungumzo Ya Pande Mbili

Baraza la Magavana limemteua Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka kuongoza mazungumzo kati ya timu ya Kenya Kwanza na timu ya Azimio la Umoja one-kenya.

 

Kulingana na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Gavana Ann Waiguru, Lusaka atakuwa miongoni mwa magavana wengine kumi wanaotarajiwa kushirikisha viongozi kutoka mirengo miwili ya kisiasa katika jitihada za kumaliza mzozo wa kisiasa unaoshuhudiwa kwa sasa nchini.

 

Wengine katika kamati hiyo ni pamoja na Anne Waiguru, Ahmed Abdlahi,Stephen Sang, Fatuma Achani,Mutahi Kahiga,Simba Arati-,Joseph Ole Lenku,Ochilllo Ayacko, na Wavinya Ndeti.

 

Kamati inalenga kushughulikia maandamano yanayoendelea na kutafuta suluhu la amani ili kuhakikisha utulivu nchini.

 

Mazungumzo ya pande mbili za Bunge kati ya kamati hizo mbili Jumanne yaligonga mwamba kufuatia kutoelewana kuhusu uanachama wa kamati ya pamoja ya pande mbili na kuanzishwa tena kwa maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio.

 

Mkutano ambao ulikuwa ufanyike Jumanne haukufaulu kwa kuwa timu ya Azimio haikufika.

 

Timu ya Kenya Kwanza imeitaka timu ya Azimio kupitia kwa Mwenyekiti Mwenza, Otiende Omollo kufikiria upya msimamo wao kwa manufaa ya Taifa na kuanza tena mazungumzo mara moja.

 

Magavana hao pia wamekiri kuwa tangu notisi ya baraza hilo mnamo Aprili, hazina ya kitaifa kufikia sasa imetoa shilingi bilioni 31 kwa kaunti ambazo ni mgao wa mwezi wa Februari.

 

Kadhalika Magavana hao wamebaini kuwa shilingi bilioni 29 bado zilikuwa zinadaiwa na kaunti zilizokusudiwa mwezi wa Machi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!