Wahalifu Wadogo 7,281 Waliachiliwa Kufikia Machi
Jumla ya wahalifu wadogo 7,281 wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali nchini wameachiliwa kufikia tarehe 30 Machi 2023.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Huduma za Urekebishaji Mary Muthoni Muriuki, hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magereza nchini.
Aidha amesema idadi kubwa ya watu kukaa ndani pia ilifanya iwe vigumu kudumisha usalama wa wafungwa na wafanyakazi wa magereza na hivyo kusababisha ongezeko la hatari ya vurugu, milipuko ya magonjwa na masuala ya afya ya akili miongoni mwa wafungwa, jambo ambalo linaweza kuzidisha changamoto zinazowakabili wafungwa.
Muriuki amezungumza hayo baada ya kuzuru magereza 76 na taasisi 4 za uangalizi kwa lengo la kubadilisha huduma za urekebishaji.
Idara ya Serikali ya Huduma za Urekebishaji pia imewasilisha ripoti elfu 6,547 za mpito ya hukumu kwa Mahakama Kuu huku wafungwa elfu 1,685 wakiachiliwa huru na kuwekwa chini ya Mpango wa uangalizi.