Moses Cheboi Miongoni Mwa Walioteuliwa Na Ruto
Rais William Ruto amefanya uteuzi wa ziada kwa serikali yake huku akiendelea kurekebisha utawala wake miezi minane baada ya kushika wadhifa huo.
Katika notisi ya gazeti la serikali ya Aprili 28, Rais Ruto amemteua aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Cheboi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Malalamiko ya Mawakili kwa muda wa miaka mitatu; uteuzi huo ulianza jana tarehe 27 Aprili 2023.
Peter Ereri Nyaga, Prof. Collins Odote Oloo, Mueni Kalola na Patrick Maina Muriuki vile vile miongoni watakaoongoza tume hiyo .
Wakili Joseph Gitonga M’limbine ataongoza Shirika la Maendeleo la Maeneo ya Chai ya Nyayo kama Mwenyekiti kwa miaka mitatu ijayo, kulingana na notisi hiyo.
Katika notisi hiyo hiyo, Jaji Mkuu Martha Koome pia alitangaza kuanzishwa kwa Sajili Ndogo ya Mahakama Kuu ya Lamu kuanzia Aprili 19, 2023.
Koome vile vile amemteua tena Dkt. Njaramba Gichuki kuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Kitaifa ya Mapitio ya Utawala wa Usafiri wa Anga kwa miaka mitatu ijayo.
Debra Ajwang, Karumba Kinyua, Kithinji Sylvia na Michoma Beth Kemunto pia wameteuliwa kuwa wanachama wa Mahakama ya Kesi za Kifedha.
Murunga Bernard Wafula Munyefy vile vile ataketi katika Mahakama ya Mizozo ya Michezo kama mwanachama kwa muda wa miaka mitano.
Koome pia amemteua Abdirahman Adan Abdikadir na Jin Mohamed Huzna kama wanachama wa Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Kisiasa kwa kipindi cha miaka sita inayoweza kurejeshwa.
Prof. Jenesio Kinyamario pia ataongoza Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbe kama Mwenyekiti kwa miaka mitatu ijayo.
Katibu wa Baraza la Mawaziri la teknolojia na mawasiliano Eliud Owalo, kwa upande wake, amemteua aliyekuwa Seneta Mteule Rose Nyamunga kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Posta la Kenya kwa muhula wa miaka mitatu.
James Wainaina, Felistus Wangari Mwangi, Simon Eric Mukhwana na David Kipkorir Kemboi pia watahudumu kama wanachama wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Maendeleo ya Maji ya Athi River hadi 2025.