Mawakili Kumi Bandia Wa Nanyuki Kufikishwa Mahakamani Leo Jumatano
Washukiwa kumi ambao wamekuwa wakijifanya mawakili na kuwalaghai wateja wasio na hatia wamekamatwa jana katika Mji wa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.
Washukiwa hao, ambao baadhi yao walikuwa wakiendesha afisi mjini walikamatwa wakati wa operesheni kali iliyofanywa kwa pamoja na maafisa wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) na afisi ya Kurugenzi ya Uchunguzi na makosa ya Jinai DCI.
Mwenyekiti wa LSK Nanyuki Joseph Mwangi alisema walifanya oparesheni ya kuwaondoa mawakili ghushi mjini humo kufuatia malalamishi mengi kutoka kwa wananchi.
Vile vile Alisema baadhi ya mawakili hao wanajifanya mawakili katika mwenendo wa kesi mahakamani huku wengi wao wakiwa wamebobea katika kuandaa mikataba wakati wa shughuli za mali, kesi za madai na urithi.
Afisa wa Upelelezi wa Jinai wa Kaunti ya Laikipia (C.C.I.O) Onesmus Towett alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao na kuongeza kuwa watafikishwa mahakamani leo hii Jumatano.
LSK sasa inawashauri wananchi dhidi ya kushirikisha huduma za mawakili bila ya kwanza kuthibitisha na afisi zao.