Home » Walimu Walioharibu Sehemu Ya Siri Ya Mwanafunzi Waachiliwa Kwa Dhamana

Walimu Walioharibu Sehemu Ya Siri Ya Mwanafunzi Waachiliwa Kwa Dhamana

Walimu watatu wa Shule ya Sekondari ya Nyabisia, eneo bunge la Bobasi waliokamatwa kwa kumjeruhi mwanafunzi korodani, wamefikishwa katika Mahakama ya Ogembo mjini Kisii, huku wengine wawili na mlinzi wakikosa kufika.

 

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 alisema walimu watano na mlinzi wa shule walimpiga vikali kiasi cha kuharibu moja ya viungo vyake vya uzazi.

 

Madaktari katika Hospitali ya Hema katika Mji wa Kisii pia walithibitisha kuwa kiungo hicho kilikuwa kimeharibiwa vibaya na kuondolewa kwa upasuaji.

 

Wakaazi wa eneo hilo wameitaka wizara ya elimu kuchukua hatua kali dhidi ya walimu wahusika ili kukabiliana na ongezeko la visa vya mateso vinavyoonekana kukithiri katika shule za kaunti ya Kisii.

 

Baada ya kumtembelea mwanafunzi huyo hospitalini, Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo, Charles Kases, aliwafahamisha wanahabari kuwa majeraha aliyopata mvulana huyo yalikuwa ya kusikitisha.

 

Kijana huyo alieleza kuwa baada ya walimu hao kubaini kuwa alikuwa na karatasi ya mtihani iliyoonekana, walimfunga kamba na kumpeleka kwenye chumba ambacho wanafunzi wengine wa shule hiyo walikitaja kuwa ni chumba cha mateso ambapo walimpiga kwa masaa mawili bila huruma.

 

Mwanafunzi huyo aliachwa na korodani inayovuja damu, na alipofikishwa hospitalini, wahudumu wa hospitali ya Hema mjini Kisii waligundua kuwa korodani lake lilikuwa limejeruhiwa.

 

Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 27, 2023

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!