Home » Kamishna Bonde La Ufa Abdi Hasaan Ataka Waliovamia Mashamba Ndabibi Kuhama

Kamishna Bonde La Ufa Abdi Hasaan Ataka Waliovamia Mashamba Ndabibi Kuhama

Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa Abdi Hassan ametoa ilani kwa maskwota wote waliovamia ardhi ya kibinafsi ya Naivasha kuhama.

 

Kamishna huyo amekiri kwamba matukio hayo yalikuwa yamechochewa kisiasa hali itaendelea kuwa mbaya zaidi iwapo haitashughulikiwa vyema.

 

Haya yanajiri huku akikiri kuwa kesi zinazoendelea mahakamani kuhusu umiliki wa mashamba yaliyovamiwa ndizo changamoto kuu ambazo maafisa wa usalama wanakabiliana nazo kwa sasa.

 

Katika wiki tatu zilizopita, maskwota zaidi ya 500 walivamia ardhi ya kibinafsi ya Ndabibi na kuanza kulima na kupanda, hivyo kuzua ghadhabu na wasiwasi kutoka kwa wamiliki.

 

Huko Mai Mahiu, makumi ya wafugaji wiki jana waliteketeza afisi za shamba la Utheri Wa Lari na kuharibu mali ya mamilioni ya pesa kutokana na mzozo wa ardhi.

 

Wakati akitoa onyo hilo, Hassan amesema wataingilia kati ili kubaini ni nani ana hati za umiliki wa kweli kwa mashamba hayo.

 

Akihutubia wanahabari baada ya kufanya mkutano wa huko Naivasha, Hassan ametoa onyo kwa maafisa wa serikali kujiepusha na mizozo ya ardhi na kudai kuwa ofisi yake inafahamu malalamiko yaliyotolewa na wakazi wa eneo hilo kuwa baadhi ya maafisa wa serikali walikuwa wakikodisha sehemu za ardhi inayozozaniwa na hivyo kusababisha hali ya sintofahamu kwa sasa.

 

Mapema wiki hii, wakulima kutoka Ndibibi, Mwana Mwireri, Kati na Kiribon walishutumu maafisa wa serikali kwa kukodisha ardhi ya zamani ya ADC licha ya ardhi hiyo kuwa na mzozo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!