Muthama: Kwa Nini Sitampokea Rais Ruto Ukambani?
Aliyekuwa mwenyekiti wa (UDA) Johnstone Muthama amedai kwamba atakuwa akisafiri nje ya nchi wakati ambapo Rais William Ruto anatarajiwa kuzuru eneo la Ukambani mnamo Aprili 16, 2023.
Huku akiifariji familia ya mwakilishi wadi wa Nguu Masumba Daniel Musau kufuatia kufiwa na mamake huko Mweini kaunti ya Makueni, Muthama amebaini kuwa hana tatizo la kumkaribisha rais wakati wa ziara yake bali atakuwa mbali na kazi ya serikali.
Matamshi hayo kutoka kwa Muthama yanajiri siku mbili baada ya ripoti kueleza kuwa kulikuwa na msuguano kati yake na Waziri wa Masuala ya Kigeni Dkt Alfred Mutua kuhusu ni nani angemkaribisha rais Ukambani.
Viongozi kutoka vyama vya Maendeleo Chap Chap (MCC) na UDA waliripotiwa kufanya mikutano sambamba kupanga jinsi ya kuwa mwenyeji wa rais huku kila upande ukitaka kuthibitisha ubabe wake.
Kulingana na Mbunge wa Kibwezi magharibi Mwengi Mutuse, Mutua ndiye kiongozi mkuu katika eneo hilo, hivyo basi mwanasiasa anayefaa zaidi kumkaribisha rais katika eneo hilo ni Waziri Mutua.
Wanasiasa wa UDA, kwa upande mwingine, Vincent Musyoka, Katibu Mwenzi wa UDA, alibainisha kuwa chama tawala kinafaa kuwa ndicho kinachompokea Rais Ruto.