KEPSA: Kenya Inapoteza Bilioni 3 Kutokana Na Maandamano
Muungano wa Sekta ya Kibinafsi ya Kenya (KEPSA) unasema kuwa nchi inapata hasara ya takriban Shilingi bilioni 3 kila siku kutokana na maandamano ya chama cha muungano cha Azimio La Umoja One-Kenya.
Kikundi cha sekta ya kibinafsi kimewasihi wanasiasa kupitia upya msimamo wao wa kisiasa na kufikiria kufuata njia mbadala za kutatua mizozo ulioainishwa katika katiba na pia kulinda haki za biashara kufanya kazi bila hofu ya kuadhibiwa kisiasa au ghasia.
Katika taarifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa KEPSA Carole Kariuki ameelezea wasiwasi wake kuhusu maandamano yanayofanyika kila Jumatatu na Alhamisi akiyataja kuwa yanarudisha nyuma ajenda ya ukuaji wa uchumi nchini.
KEPSA pia imetoa wito kwa maafisa wa kutekeleza sheria kuzingatia raia na kutopendelea upande mmoja na kuhakikisha ulinzi sawa wakenya wote.