Home » Takriban Watu 21 Wamethibitishwa Kufariki Katika Ajali Ya Feri

Vikosi vya upekuzi nchini Gabon vimefanikiwa kupata maiti za abiria 15 wa feri iliyozama katika pwani ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi wiki iliyopita, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 21.

 

Feri ya Esther Miracle ilikuwa imebeba abiria 161 kutoka Libreville kuelekea Port-Gentil ilizama karibu na kijiji cha pwani cha Nyonie mnamo Machi 9.

 

Mamlaka ilithibitisha vifo sita siku ya Jumatatu na bado walikuwa wakitafuta watu 31 waliopotea.

 

Ndege za jeshi la anga na timu za kupiga mbizi zilikuwa zimetumwa kufanya shughuli za utafutaji kila siku.

 

Mkuu wa shughuli za uokoaji Bekale Meyong alisema kwenye runinga ya serikali kwamba watu 124 wameokolewa na 21 walithibitishwa kufariki baada ya miili 15 zaidi kuvuliwa kutokana na ajali hiyo ya meli.

 

Magari ya kubebea wagonjwa yamepeleka miili hiyo kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti na shughuli za kuwatafuta zinaendelea, aliongeza.
Serikali bado haijazungumzia sababu za tukio hilo.

 

Ripota wa shirika la habari la Reuters katika bandari ya Libreville aliona miili hiyo ikishushwa kutoka kwenye boti kwenye mifuko ya miili. Baadhi ya jamaa walikimbia kujaribu kuwatambua kabla ya polisi kuzuia kuingia.

 

Mamia ya watu wamekuwa wakikesha katika bandari ya Libreville tangu feri hiyo ilipozama katika kuonyesha mshikamano kusubiria jamaa wao.

 

Wakosoaji wa serikali ya taifa hilo wanaishutumu kwa kuchelewa kutoa majibu na kwa kupunguza ukubwa wa tukio hilo, wakisema meli hiyo ilikuwa na abiria zaidi ya ilivyofichuliwa.

 

Feri mara nyingi hulemewa nchini Gabon, na kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa kuwa meli hiyo ililemewa na magari, mifugo na bidhaa nyinginezo.

 

Msemaji wa serikali Yves Fernand Manfoumbi ameliambia shirika la habari moja kwa njia ya simu kuwa hana taarifa wala maoni yoyote kuhusu madai hayo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!