Home » Kijana Wa Miaka 22 Auawa Na Kiboko Kajiado

Mwanamume mwenye umri wa miaka 22 amefariki na mwingine kulazwa katika hospitali ya Magadi Soda baada ya kushambuliwa na kiboko eneo la Shompole, Kajiado Magharibi.

 

Kisa hicho kilitokea baada ya watu hao kwenda kuvua samaki katika mto Ewaso Nyiro kabla ya kiboko huyo kumpiga na kumuua mmoja na kumwacha mwingine na majeraha mabaya.

 

Visa vingi vya mizozo kati ya binadamu na wanyama pori vimeshuhudiwa katika kaunti ya Kajiado haswa wakati huu ambapo jamii inashuhudia ukame mkali.

 

Lazarus Saigilu, ambaye ni mwenyekiti wa wazee wa kijiji amesema kuwa watu sita wamefariki dunia katika kipindi cha mwaka mmoja kutokana na uvamizi wa kiboko.

 

Kulingana na Saigilu, binadamu na wanyama pori hung’ang’ania maji yanayopunguza na kusababisha migogoro kati yao.

 

Chifu wa eneo la Shompole Denis Kuyia amesema kuwa mzozo wa wanyamapori wa binadamu ni tatizo la kawaida na lililokita mizizi katika eneo hilo.

 

Amewataka washikadau na maafisa kutoka idara ya wanyama pori kuchukua hatua na kuwafidia wakaazi.

 

Katika kisa kingine, mzee wa makamo kutoka Oloorkunono wadi ya Mosiro anapigania maisha yake kule Narok baada ya kushambuliwa na tembo.

 

Mwanamume huyo anasemekana kupata majeraha mabaya baada ya tembo huyo kumpiga tumboni.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!