Wadau Wapinga Mapendekezo Ya Ongezeko La Ada Za Masomo Ya Chuo Kikuu
Baadhi ya wadau wa elimu maeneo ya Nyanza wamepinga mipango ya serikali ya kuongeza karo za elimu ya vyuo vikuu.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu wa Elimu ya Baada ya Shule ya Msingi Kenya (Kuppet) Akelo Misori, wabunge Tom Odege wa (Nyatike) na Adipo Okuome wa (Karachuonyo) wamesema pendekezo hilo litaumiza wanafunzi kutoka familia maskini kwa kuwanyima fursa ya kupata elimu ya juu.
Marekebisho ya jopokazi la Rais William Ruto kuhusu elimu lilipendekeza kuongezwa kwa ada zinazolipwa katika taasisi za elimu ya juu kama njia ya kuzisaidia taasisi hizo kuendelea kujiendesha kifedha.
Jopokazi lililowasilisha ripoti yake kwa Rais William Ruto pia limependekeza msururu wa hatua zinazolenga kuboresha ubora wa elimu ya juu nchini.
Aidha, baadhi ya washikadau wa elimu wanataka serikali kutotekeleza mapendekezo hayo kwa misingi kwamba yatawaweka kando watoto wanaotoka katika familia maskini.
Kutokana na hali hiyo, viongozi hao wanaitaka serikali kubatilisha utekelezaji wa pendekezo hilo wakisema itafanya elimu ya chuo kikuu kuwa ghali hasa kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini.
Misori amedai kuwa karo za kupandishwa zitasababisha mzigo mkubwa kwa wazazi na kuwazuia watoto wao kupata elimu katika vyuo vya juu.
Vile vile, amebainisha kuwa wazazi tayari wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kiuchumi hivyo wanapaswa kuepushwa na karo zinazoongezwa.
Katibu mkuu wa Kuppet amewataka wabunge kutunga sheria inayozuia serikali kuongeza karo kwa vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi.
Kwa upande wake, mbunge Odege amesema kufanya hivyo, kutasababisha kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa elimu ya juu kwa wanafunzi wengi ambao familia zao zina changamoto ya kifedha.
Mbunge huyo ameonya kuwa ni asilimia kumi pekee ya wanafunzi wanaweza kumudu karo iliyoongezwa katika vyuo vikuu kwa vile wengi wao wanatoka katika familia maskini na kuahidi kuwasilisha hoja bungeni ili kuishinikiza serikali kutoongeza ada katika vyuo vikuu.
Viongozi hao wamezungumza wakati wa sherehe za mahafali ya tano ya Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi ya Mawego katika eneo bunge la Karachuonyo mwishoni mwa juma.
Jumla ya wanafunzi 2,462 walihitimu mafunzo ya ufundi, kupata vyeti, stashahada ya juu.