Acha Kulaumu Uongozi Wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta asema Sabina Chege

Mbunge mteule Sabina Chege amepinga Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kuendelea kulaumu uongozi uliopita.
Akizungumza wakati wa mahojiano na runinga moja humu nchini, Chege alitoa changamoto kwa rais Ruto na Gachagua kuzingatia majukumu yao kama viongozi wa nchi na kukoma kumlaumu rais wa zamani Uhuru Kenyatta.
Chege amewaambia wawili hao kuiga mfano wa rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki ambaye aliacha historia kwa kuendeleza nchi bila kulaumu utawala uliopita wa marehemu Daniel Moi.
Mbunge huyo amewataka Wakenya kumheshimu rais mstaafu kenyatta kwani pia aliahidi kuhudumia kila mtu licha ya tofauti za awali.
Aidha alibainisha kuwa wakati wa mkutano wa ikulu na Ruto, alitangaza kuwa amesamehe kila mtu aliyemdhulumu.
Akizungumzia suala la handisheki, Chege alidai kuwa hatua ya rais Ruto na upinzani ni tofauti na makubaliano ya Uhuru na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 2018.
Aliyekuwa mwakilishi wa wanawake wa Murang’a huyo alimtaka Uhuru kusimama kidete na chama cha Jubilee kabla ya kusikiliza siasa za watu wengine.
Akipuuzilia mbali madai ya kuvunjilia mbali upinzani na Ruto, Chege alisema kuwa hakuna mipango ya kuvunja chama chochote na kubainisha kuwa lengo lao ni kutaka chama kisimame kidete na chini ya kiongozi wao kama ilivyokuwa katika mifumo mingine ya kisiasa.
Akizungumzia tishio la katibu jeremiah Kioni la kupoteza Nafasi hiyo, Chege alibainisha kuwa hatasita kujisalimisha ikiwa chama kitahisi wanataka kumbadilisha na kuchukua mtu mwingine.